Saturday, May 21, 2011

MBUNGE ATOA MABASI KUBEBA WANAFUNZI BURE.. GAZETI LA MWANANCHI TAREHE 21-3-2011

TATIZO la kuchelewa shuleni kwa wanafunzi wa shule za sekondari wanaosoma Kando ya Manispaa ya Mtwara-Mikindani, limefika mwisho baada ya mbunge wa jimbo hilo, Hasnein Murji kutoa mabasi mawili kwa ajili ya kusafirisha wanafunzi hao.
Mabasi hayo yatasafirisha wanafunzi bure kwa lengo la kuwawezesha kuwahi kwenda na kurudi shuleni hali itakayoongeza ushiriki wa wanafunzi katika masomo hivyo kukuza taaluma shuleni.
Akizungumza na Mwananchi jana mjini Mtwara, mbunge huyo  alisema kati ya mabasi hayo, moja litasafirisha wanafunzi kutoka kituo kikuu cha mabasi hadi Naliendele umbali wa zaidi ya kilomita 10, ambalo litabeba wanafunzi wanaosoma shule za sekondari za maeneo hayo.
Alifafanua kuwa basi lingine litaanza safari zake kituo kikuu cha mabasi cha mjini hapa na kuelekea Mikindani umbali wa zaidi ya kilomita nane na kwamba msaada huo pia unalenga kumpunguzia mzazi gharama za kusomesha.
“Nimetoa mabasi mawili kwa ajili ya kusafirisha wanafunzi, basi linalokwenda Naliendele tayari limeanza safari, wakati gari la Mikindani linataraji kuanza kutoa huduma hiyo mwishoni mwa wiki hii, huu ni utekelezaji wa ahadi yangu niliyoitoa wakati wa kampeni” alisema Murji
Aliongeza kuwa “Ni imani yangu kuwa wazazi hawataniangusha, pesa waliyokuwa wanaitumia kwa ajili ya nauli sasa waitumie kwa kuwatimizia mahitaji mengine ya shule watoto wao ili tuweze kufikia lengo la kukuza taaluma, haya ni mabasi aina ya ‘Coaster’ ambayo awali nilikuwa nayatumia kwa ajili ya kusafirisha abiria”, alisema.
Baadhi ya wanafunzi wanaosoma Shule ya Sekondari ya Naliendele walielezea kufurahishwa kwao kwa utekelezaji wa haraka wa ahadi hiyo kwani imewaondolea adha ya kusafiri kwa baiskeli, miguu kwenda na kurudi hivyo kuathiri ushiriki wao katika masomo.
“Tulikuwa tunaingia darasani  saa tatu na wakati mwingine saa nne, wakati huo tayari walimu wanakuwa wameingia darasani, hata kwa wale wenye pesa usafiri ulikuwa wa shida sana, kwa hili tunamshukuru sana mbunge wetu” alisema Jasmini Abdallah
Kwa upande wao wananchi wa jimbo hilo pia walimpongeza Murji kwa uwamuzi wake huo ambao walisema utawanufaisha wananchi wote wa jimbo hilo na kutoa wito kuendelea na utekelezaji wa ahadi zingine.
“Mbali ya faida anayopata mzazi kwa kupunguziwa gharama za kusomesha, wasomi watakaotoka kwenye shule hizo watainufaisha Mtwara na Taifa kwa ujumla, nampongeza mbunge katika hili na kumtaka aendelee na utekelezaji wake wa ahadi zingine” alisema Issa Msuo Mwenyekiti wa Kijiji cha Mkangala Kata ya Naliendele.

No comments:

Post a Comment